Lugha ya Kiswahili Katika Bahari Tete na Tata
Licha ya hadhi na umaarufu wa Kiswahili ndani na nje ya nchi, bado lugha hii inakumbwa na matatizo yasiyomithilika ki-dhana na ki-matumizi. Kwa muda mrefu, baadhi ya watu wamekuwa wakinasibisha Kiswahili na dini ya Kiislamu na hivyo kuzua mgawanyiko kwa misingi ya kiimani miongoni mwa wasemaji wake.
Pia kunao upinzani mkubwa kutoka kwa lugha ambazo zimekwisha kujitanua kimatumizi kote duniani kama vile Kiingereza, Kifaransa, Kihispania, Kijerumani, Kichina, Kireno na Kiarabu na lugha nyinginezo. Watumizi au watu wenye asili ya lugha hizo wanakipiga vita Kiswahili wakihofia kuwa wasipofanya hivyo kitaishia kuzimeza lugha zao katika siku za halafu.
Kudharauliwa kwa lugha ya Kiswahili na kupigiwa chapuo kwa lugha nyinginezo za kigeni kwamba ndizo pekee zinazofaa kutumiwa katika shughuli mbalimbali za kiuchumi kwa kuwa zina hadhi ni changamoto kubwa.Kuna kasumba mbaya na mtazamo hasi kuhusu Kiswahili na ambao unawafanya Wakenya kukitukuza na kushabikia zaidi Kiingereza kwa kutojua kuwa Kiswahili ni sawa na lugha nyinginezo tu kihadhi.
Huku tukichunguza nafasi ya Kiswahili katika mfumo wa elimu nchini Kenya, ni vyema tukumbuke kuwa, mfumo wa elimu wa nchi yoyote iwayo unaotegemea lugha za kigeni hasusan lugha ya mkoloni huishia tu kuendeleza maadili ya kigeni na utegemezi (Mbaabu 1996) Kwa sababu ya utandawazi na maendeleo ya sayansi na teknolojia, lugha huathiriana duniani kote. Lugha za kigeni katika mfumo wa elimu hunuia kuendeleza mila na desturi za kigeni ambazo nyingi yazo haziambatani wala kulingana na matarajio na mahitaji ya kimaendeleo ya nchi. Kwa misingi hii, ni muhimu kwa wataalamu, watafiti na wasomi wa Kiswahili kujaribu kuipa nafasi inayostahili lugha hii katika mfumo wetu wa elimu ili kuustawisha mustakabali wake.
Njia mojawapo ya kufanikisha lengo hili bila shaka ni kuwepo kwa vitabu vya Kiswahili sanifu vinavyotumiwa katika mfumo wa elimu. Uandishi wa vitabu huchangia pakubwa katika kufanikisha malengo ya elimu katika nchi yoyote ile. Kulimatia kwa maamuzi ya sera ya kukipa Kiswahili hadhi kuwa lugha ya kufundishia na lugha funzwa inayotahiniwa katika tasnia zote za elimu ni pigo kubwa kwa maendeleo ya Kiswahili.
Hali ya Wakenya kuwa nyuma katika kufanya tafiti mbalimbali kuhusu vipengele muhimu vya fasihi na isimu katika Kiswahili ili kuona ni jinsi gani tunaweza kufunguka kiakili na kufahamu umuhimu wa kuwa na Kiswahili ni kisiki kingine.
Uchumi mdogo wa nchi yetu unakwamiza pakubwa maendeleo ya haraka ya Kiswahili kote duniani. Kwa kuwa nchi inashindwa kuzalisha wataalamu wengi wa lugha hii, pia inashindwa kutafsiri maandiko kutoka kwa lugha nyingine hadi kwa Kiswahili kwa hofu ya gharama ya juu na shughuli nzima ya kuunda asasi na taasisi za kuzizamia taaluma za Kiswahili.
Wakenya wanakosa moyo wa kuthamini na kujali tamaduni zao. Ni bayana kuwa Wakenya hawana mwao kuwa Kiswahili ni lugha inayotangaza na kutambulisha utamaduni na utaifa wetu. Hali hii imepelekea wao kuthamini sana itikadi za Kimagharibi. Ukengeushi huu umewafanya kuyaiga matendo, mil ana itikadi za kigeni. Huu umeishia kuwa mkasa mkubwa ambao umekitanza Kiswahili katika juhudi za kujitanua kihadhi.
Vinginevyo, kwa muda mrefu, kumekuwa na dhana potovu kuwa Kiswahili ni lugha duni. Hali hii imewafanya watu kutaka kujifunza Kiingereza na lugha nyingine za kigeni huku wakipuuza Kiswahili ambacho ni kitambulisho chao.
Kwa upande wa matumizi ya Kiswahili, kumekuwa na tatizo la kutumiwa visivyo katika Nyanja za kimatamshi na kimaandishi. Ni Jambo la kusikitisha na kuatua moyo kuona kuwa miaka mingi baada ya kusanifishwa kwa Kiswahili, bado watumizi wake wanakisema na kukiandika visivyo. Ni kinaya kikuu kuwa baadhi ya makosa haya hufanywa na taasisi ambazo hata ndizo zingetarajiwa kuendeleza matumizi sahihi ya Kiswahili. Mwito wangu kwenu, ni kuwa sote kama Wakenya wazalendo tuwe katika mstari wa mbele katika kupigania kuinua hadhi ya lugha hii ajuadi na faridi ya Kiswahili.